Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2018 - 2019
Abstract
Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2018/19 ni wa tatu katika utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, 2016/17 – 2020/21. Malengo mahsusi ya Mpango huu ni: (a) Kuendeleza kasi ya ukuaji wa uchumi kwa kuongeza matumizi ya fursa na majaliwa ya kipekee ya nchi kwa tija; (b) Kuimarisha kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Miaka Mitano, hasa kwa kutanzua changamoto za upatikanaji wa fedha na mitaji, ardhi na maeneo ya uwekezaji, na kuimarisha mipango miji na maendeleo ya makazi; (c) Kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani; (d) Kupanua fursa kuwezesha wananchi wengi kushiriki katika uwekezaji na uendeshaji biashara ili kuongeza uwezo wa nchi na wananchi kupambana na umaskini; (e) Kuimarisha ustawi na maendeleo ya jamii kwa kuongeza upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji na kinga kwa jamii na kaya maskini; (f) Kuongeza idadi ya rasilimali watu yenye ujuzi na weledi unaohitajika katika uendeshaji wa uchumi wa viwanda na
kuimarisha upatikanaji wa teknolojia na ubunifu na hivyo kujenga uwezo wa nchi kushindana kibiashara; na (g) Kuongeza uzalishaji katika sekta asili (primary production) ili kukidhi mahitaji na usalama wa chakula na upatikanaji wa mazao ghafi kwa uzalishaji viwandani kwa bei itakayowezesha ushindani kimataifa